Jumamosi 25 Julai 2026 - 23:43
“Khamenei” ni jina lililowakusanya pamoja wanaoitafuta haki kutoka kila pembe ya dunia

Hawza/ Mratibu wa Bunge la Kitaifa la Dini nchini India amesema: “Mapenzi yetu kwa Shahidi Ayatullah al-Udhma Khamenei (ra) yanavuka mipaka ya siasa; yanafafanuliwa kwa kuenzi ubinadamu. Alikuwa shujaa mkubwa ambaye jina lake liliwakusanya pamoja wanaoitafuta haki kutoka pande zote nne za dunia.”

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Goswami Sushil Ji Maharaj, Mratibu wa Bunge la Kitaifa la Dini za India, ambaye alisafiri kwenda Iran kushiriki katika hafla ya mazishi ya Ayatullah Khamenei (ra), alisema kuhusu shakhsia ya Kiongozi huyo Shahidi: “Kinyume na baadhi ya propaganda zinazoenezwa, Ayatullah Khamenei (ra) hakuwaza nchi yake pekee, bali alikuwa na shauku ya kuona amani, utulivu na mustakabali mwema wa wanadamu wote, na daima alisisitiza mazungumzo badala ya vita.”

Goswami Sushil Ji Maharaj alieleza kuwa; kitendo cha kumuua kwa njama kiongozi wa kidini ni kinyume na misingi ya kibinadamu na hata sheria za vita, akaongeza kusema: “Katika historia kumekuwa na vita vingi, lakini hata vita vina kanuni zake. Kumlenga na kumuua kishahidi kiongozi wa kidini ni kitendo kisichokubalika. Ikiwa leo kiongozi mmoja wa kidini analengwa, kesho viongozi wengine wa dini mbalimbali wanaweza pia kukabiliwa na tishio kama hilo. Ndio maana dini zote za Tauhidi zinaomboleza kupaa kishujaa kwa Kiongozi Shahidi wa Iran.”

Kumuua kwa njama kiongozi wa kidini ni kinyume na misingi yote ya maadili

Mwanazuoni huyo mashuhuri wa kidini kutoka India, huku akiikosoa kwa njia ya mafumbo Marekani na nchi za Magharibi, alisema: “Kuwa dola kubwa hakumaanishi tu kuwa na silaha na vifaa vya kijeshi. Dola kubwa ya kweli ni ile inayoulinda ulimwengu, si ile inayowaua wale wanaotafuta amani na utulivu kwa ajili ya watu. Kuelezea au kuhalalisha uhalifu wa aina hii kunamaanisha kwamba ubinadamu umetoweka.”

Pia aligusia kuuawa kwa watoto katika vita pamoja na wanafunzi wa Minab, akisema kuwa matukio hayo ni dalili ya kuporomoka kwa maadili ya kibinadamu, na akaongeza: “Wale wanaojitahidi kulinda heshima ya mwanadamu wanapaswa kuungwa mkono, si kuwa walengwa wa vitendo vya kikatili.”

Mratibu wa Bunge la Kitaifa la Dini za India, akisema kwamba Ayatullah Khamenei (ra) alikuwa akiwaunga mkono wale waliopigania kuhifadhi maadili na kusimama dhidi ya wale wanaoharibu ubinadamu, alisisitiza: “Ndiyo sababu sisi tunampenda sana na tunavutiwa na fikra pamoja na itikadi yake. Tutaendelea kutembea katika njia yake, na Inshaallah hatutaruhusu maneno na fikra zake zipotee. Badala yake tutazidumisha zikiwa hai, na kwa kushirikiana pamoja tutaendeleza njia hii yenye nuru.”

Goswami Sushil Ji Maharaj alisema kuwa ujumbe wa Bunge la Dini za India ulikuwa miongoni mwa makundi ya kwanza kufika Iran kwa ajili ya kutoa heshima, na akaeleza: “Sisi hatukuja kwa niaba ya serikali yoyote wala taasisi yoyote ya kisiasa, bali tumekuja kwa niaba ya wanaoitafuta haki na kwa ajili ya kutoa heshima kwa shakhsia ambayo kwa imani yetu ilijitolea kuutetea ubinadamu.”

Sisi ni waenezaji wa njia ya Imam Khamenei (ra)

Akirejelea historia ndefu ya uhusiano wake na Iran pamoja na Kituo cha Utamaduni cha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini New Delhi, alieleza kuwa uhusiano kati ya Iran na India ni wa kihistoria na wenye mizizi imara, akiongeza:

“Iran na India tangu zamani zimekuwa na mafungamano ya pamoja ya kiutamaduni na ya ustaarabu, na tunapaswa kujitahidi kuyaimarisha zaidi mahusiano haya. Tunatembelea mara kwa mara Kituo cha Utamaduni cha Iran mjini New Delhi, na tumekuwa na uhusiano nacho kwa miaka mingi.”

Mwanazuoni huyo mashuhuri katika mazungumzo ya baina ya dini, katika hitimisho la hotuba yake alisisitiza: “Ujumbe wa amani na mazungumzo ambao Ayatullah Khamenei (ra) alikuwa akiuhimiza ndio ujumbe tunaoufuata sisi pia.

Nina umri wa miaka 82, na licha ya umri huo bado nasafiri katika nchi mbalimbali nikiwa naeneza ujumbe mmoja tu; nao ni ujumbe ule ule wa amani ambao Ayatullah Khamenei (ra) alikuwa akiutangaza, na ndio ujumbe ambao sisi pia tunaamini.”

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha